Search the region
22344 stories
TEITI YAZITAKA TAASISI KUTOA TAARIFA ZA MAPATO KABLA YA SHERIA KUCHUKUA MKONDO
Na Janeth Raphael - MichuziTv Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), imezitaka taasisi zinazowajibika kuwasilisha taarifa za mapato yatokanayo na rasilimali hizo kwa wakati, ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za Taifa. Wito huo umetolewa leo Septemba 22, 2026, mkoani Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI, Balozi Wilson Masilingi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesisitiza umuhimu wa taasisi kutekeleza wajibu wao wa kisheria kwa kuwasilisha taarifa zinazohitajika kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao. Balozi Masilingi amesema TEITI ina jukumu la kusimamia na kuhakiki taarifa za mapato yanayotokana na shughuli za madini, mafuta na gesi asilia, pamoja na kufuatilia iwapo mapato hayo yanawasilishwa kwa usahihi na hatimaye kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi. Amesema ushirikiano wa taasisi zinazohusika ni muhimu katika kufanikisha jukumu hilo, hususan kwa kuhakikisha taarifa za mapato na malipo yanayotokana na sekta za rasilimali zinawasilishwa kwa wakati, kwa usahihi na kwa uwazi. Miongoni mwa taasisi zinazowasilisha taarifa na kuwa chini ya ufuatiliaji wa TEITI ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tume ya Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Ofisi ya Msajili wa Hazina. Taasisi nyingine ni mifuko ya hifadhi ya jamii, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA). Hatua hiyo inalenga kuimarisha mfumo wa uwazi katika sekta za madini, mafuta na gesi asilia, kwa kuwezesha mamlaka husika kupata taarifa sahihi za mapato yanayotokana na rasilimali hizo na kufuatilia namna yanavyokusanywa na kusimamiwa kwa manufaa ya Taifa.
Tue, 22 Sep 2026 12:02:09 +0000DKT. MWIGULU: UWEZESHAJI WA WANAWAKE NI UWEKEZAJI KATIKA AFYA MOJA
▪️︎ Aeleza hatua za Tanzania kuwawezesha wanawake katika kilimo WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba alisema uwezeshaji wa wanawake wakulima ni uwekezaji katika utekelezaji wa dhana ya Afya Moja, kutokana na nafasi yao katika uzalishaji wa chakula, ufugaji, lishe, afya ya mifugo, usalama wa chakula na utunzaji wa mazingira. “Wanawake hawapo pembezoni mwa mifumo ya chakula na kilimo; wako katikati yake. Kuwawezesha wanawake ni uwekezaji si katika kilimo pekee, bali pia katika Afya Moja,” alisema. Waziri Mkuu alisema hayo jana (Jumatatu, Septemba 21, 2026) wakati akizungumza katika kikao cha ngazi ya juu kuhusu Mwaka wa Kimataifa wa Mwanamke Mkulima 2026, chenye mtazamo wa Afya Moja, kilichofanyika katika Kituo cha Sheikh Zayed, Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma, Italia. Alisema Tanzania inaongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Rais wa kwanza mwanamke katika historia ya nchi, akieleza kuwa wanawake wana nafasi kubwa katika uzalishaji wa chakula na maendeleo ya kilimo. Dkt. Mwigulu alisema pamoja na mchango huo, wanawake bado wanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa ardhi, fedha, teknolojia, huduma za ugani, masoko na nafasi za kufanya maamuzi. Alisema Serikali inaendelea kuwawezesha wanawake na vijana kupitia Mpango wa Kujenga Kesho Bora (BBT), ambao unalenga ifikapo mwaka 2030 kuunda ajira milioni 1.6, kusaidia biashara za kilimo 200,000 zinazomilikiwa na vijana na wanawake na kunufaisha takribani watu milioni 10 katika vijiji 12,000. Alisema hadi Juni 2026, Sh. bilioni 1.59, sawa na takribani Dola za Marekani 601,000, zilitolewa kwa wanufaika 47, ambapo 17, sawa na asilimia 36, walikuwa wanawake. Aidha, alisema BBT imesambaza maafisa ugani vijana 2,282 katika mikoa 22, ambao wamewafikia takribani wakulima wadogo 765,600 katika vijiji 5,856 kwa kutoa huduma za ushauri na kuelimisha kuhusu kanuni bora za kilimo. Alisema Serikali pia inaendelea kuwekeza katika miradi ya maji na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ambapo hadi sasa visima 395 vinavyotumia nishati ya jua na kuzingatia teknolojia inayokabiliana na mabadiliko ya tabianchi vimechimbwa katika vijiji 234 vya wilaya 45 nchini. Dkt. Mwigulu alisema Serikali pia inawawezesha wanawake na vijana kuhamia kutoka uzalishaji wa awali na kushiriki katika shughuli zenye thamani kubwa zaidi, ambapo vijana na wanawake 408 wamepatiwa mafunzo kuhusu uongezaji thamani wa mkonge, hatua inayolenga kuimarisha ushiriki wao katika minyororo ya thamani ya kilimo na kuongeza fursa za kipato. “Uwekezaji huu si uwekezaji wa kilimo pekee; ni uwekezaji wa Afya Moja,” alisema. Alisisitiza kuwa wanawake wanapaswa kutambuliwa si kama wanufaika pekee, bali kama wazalishaji, wabunifu, wajasiriamali na wafanya maamuzi, huku akitoa wito wa kuimarisha sera na uwekezaji unaowawezesha kupata ardhi, fedha, teknolojia, maji, huduma za ugani na masoko. Dkt. Mwigulu alisema Tanzania iko tayari kushirikiana na FAO na wadau wengine kuhakikisha Mwaka wa Kimataifa wa Mwanamke Mkulima unaacha matokeo yanayoonekana hata baada ya mwaka 2026. Akichangia uzoefu wake katika jopo hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI), Dkt. Appolinaire Djikeng, alisema wanawake, hususan wanawake wafugaji, tayari wana nafasi muhimu katika utekelezaji wa dhana ya Afya Moja, akieleza kuwa wanafanya maamuzi ya kila siku kuhusu afya ya mifugo, usalama wa maji, lishe ya kaya na matumizi ya rasilimali, hivyo kutotambuliwa kwao kunaweza kudhoofisha juhudi za kudhibiti magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. Dkt. Djikeng pia alisema uchambuzi wa masuala ya kijinsia haupaswi kuwa jambo la kuongezwa mwishoni katika utekelezaji wa Afya Moja, bali unapaswa kuwa sehemu ya mipango tangu mwanzo, huku akisisitiza umuhimu wa kutenga rasilimali za kutosha, ikiwemo fedha na watu, ili kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi na kufanya maamuzi.
Tue, 22 Sep 2026 12:10:44 +0000MAKUNDI MAALUM KUSHIRIKI MIRADI YA MAFUTA NA GESI ASILIA
Na Mwandishi Wetu, Lindi WATU wenye mahitaji maalum mkoani Lindi wametakiwa kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ikiwemo sekta ya mafuta na gesi asilia. Wito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Lindi, Alusaria Mushi, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Adam Malima, wakati akifungua kongamano la siku moja la ushirikishwaji wa wazawa jumuishi. Kongamano hilo limeandaliwa na Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Sauti ya Wanawake Wenye Ulemavu Tanzania (SWAUTA). Mushi amesema makundi hayo hayapaswi kujiona yameachwa nyuma, bali yanapaswa kutambua nafasi ya Kanda ya Kusini katika kuchangia ukuaji wa uchumi na kutumia fursa zinazotokana na miradi mbalimbali inayotekelezwa katika eneo hilo. Amesema awali miradi ya Serikali ilikuwa ikibainisha mahitaji ya wananchi na kuyafanyia kazi, lakini kwa sasa wananchi wana wajibu wa kuibua mahitaji yao ili Serikali iweze kuhakikisha makundi yote yanahudumiwa kwa usawa. Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Nyangi, amesema mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali, wakiwemo watu wenye mahitaji maalum, wanawake, vijana na wazee. Amesema lengo ni kuhakikisha makundi hayo yanapata fursa ya kushiriki na kunufaika na miradi ya mafuta na gesi asilia nchini. “Katika utekelezaji wa miradi, kila mtu ana nafasi yake ya kushiriki na kunufaika. Hata kama kuna wawekezaji kutoka nje, wazawa wana nafasi ya kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na miradi hiyo,” amesema Nyangi. Aidha, ameyataka makundi hayo kuwa na biashara zilizosajiliwa ili yaweze kushiriki katika fursa zitakapotangazwa katika maeneo yanayotekelezwa miradi, hususan mkoani Lindi. Kongamano hilo la siku moja lilikuwa sehemu ya maandalizi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Viziwi, ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Kilimanjaro. Katika kuunga mkono maadhimisho hayo, PURA imegharamia ushiriki wa watu watano kutoka CHAVITA Wilaya ya Kibiti pamoja na kugharamia vifaa vya kusaidia usikivu.
Tue, 22 Sep 2026 14:05:01 +0000UNGA 2026: TANZANIA YAIHAKIKISHIA DUNIA UZALISHAJI WA DAWA NA KUBORESHA AFYA AFRIKA
Na John Mapepele – WAF New York WAZIRI wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Tanzania itaendelea kuweka kipaumbele katika kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa, bidhaa za afya na vifaa tiba, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje, kuimarisha usalama wa afya nchini na barani Afrika kwa ujumla. Mhe. Mchengerwa amebainisha hayo leo, jijini New York, Marekani, wakati akizungumza katika kikao cha ‘Sustaining Sierra Leone’s Triple Zero Gains Through 2028’, ambapo ameiwakilisha Tanzania akiambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Grace Magembe katika mjadala kuhusu namna ya kudumisha mafanikio yaliyopatikana Sierra Leone katika kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kuongeza huduma za chanjo. Kikao hiki ambacho kimeratibiwa na Serikali ya Sierra Leone kinafanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) katika kikao cha 81 (UNGA 81), unaowakutanisha wawakilishi wa nchi zote 193 wanachama wa UN na kila nchi ina kura moja ambapo kwa Tanzania, Makamo wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi anamwakilisha Rais, Mhe Rais Samia Suluhu kuongoza ujumbe wa Tanzania. Akizungumza katika mkutano huo Mhe.Mchengerwa amefafanua kuwa Tanzania inaunga mkono kikamilifu Mpango wa Umoja wa Afrika wa AU Champion Roadmap 2026–2030 unaolenga kufikia malengo ‘zero tatu’, ambayo ni kutokuwepo kwa uzazi wa nyumbani na usio na wataalamu, kutokuwepo kwa vifo vya mama na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika, pamoja na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo. “Tanzania inajivunia kuwa na Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika katika ajenda hii. Chini ya uongozi wake, tunaunga mkono kikamilifu AU Champion Roadmap 2026–2030 na Zero tatu,” amesisitiza Mhe. Mchengerwa. Aidha, ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha huduma za afya zinapatikana jirani na wananchi wote nchi nzima pia Serikali inaimarisha mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote na kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za afya ya mama na mtoto na kuwalinda wananchi dhidi ya gharama kubwa za matibabu. Aidha, Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutumia vyanzo mbalimbali vya fedha katika kuimarisha sekta ya afya, ikiwemo ubia kati ya Serikali na sekta binafsi, ufadhili wa moja kwa moja wa vituo vya kutolea huduma za afya, mifumo ya malipo ya kielektroniki, tozo zinazolenga bidhaa maalum pamoja na kuendeleza huduma za utalii tiba, huku ikiendelea kuongeza mgao wa bajeti kwa huduma za afya ya msingi na huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga. Akizungumzia umuhimu wa uzalishaji wa ndani, amesema Afrika hutumia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 28 kila mwaka kununua dawa na bidhaa za afya, huku sehemu kubwa ya mahitaji hayo ikitoka nje ya bara hilo, jambo alilosema linaweka mifumo ya afya katika hatari ya kukumbwa na changamoto za misukosuko ya minyororo ya usambazaji na mabadiliko ya bei katika soko la kimataifa. Amesema Tanzania imeweka uzalishaji wa ndani wa dawa, bidhaa za afya, vifaa tiba na vifaa vya hospitali kuwa kipaumbele cha kitaifa, akisisitiza kuwa hatua hiyo si suala la uchumi pekee bali pia ni msingi wa kuimarisha usalama wa afya kwa kuhakikisha vituo vya kutolea huduma vinaendelea kuwa na mahitaji muhimu hata pale kunapokuwa na changamoto katika minyororo ya usambazaji duniani. Waziri Mchengerwa ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika na washirika wa maendeleo kuunganisha nguvu katika uwekezaji wa sekta ya afya, uhamishaji wa teknolojia na sera za viwanda ili kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za afya barani Afrika, huku akisisitiza umuhimu wa kujenga minyororo ya thamani ya kikanda, kuimarisha mamlaka za udhibiti na kuunga mkono ubunifu unaozalishwa barani Afrika. "Tanzania inaendelea kuhakikisha huduma muhimu za afya zinapatikana ndani ya umbali usiozidi kilomita tano kutoka kwa kila jamii, huku hospitali za rufaa zikitumika zaidi kwa wagonjwa wenye mahitaji ya huduma maalum" amesisitiza Mhe. Mchengerwa Viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya hii hutumia jukwaa hili kueleza misimamo na vipaumbele vyao kuhusu masuala ya kimataifa. Katika mkutano wa mwaka huu mambo yanayojadiliwa ni pamoja na amani na usalama, vita na migogoro, mabadiliko ya tabianchi, AI, afya ya dunia , maendeleo na SDGs. Kaulimbiu ya UNGA 81 ni (Restoring Trust, Managing Transformation), Kurejesha Imani, Kusimamia Mabadiliko.
Tue, 22 Sep 2026 14:21:28 +0000TAMASHA KUBWA LA SANAA NA UTALII KUUNGANISHA VIJANA NA KUFUNGUA FURSA ZA AJIRA ARUSHA.
Na Karama Kenyunko, Michuzi TV VIJANA,Wasanii na Wadau wa Sanaa na Utalii wanatarajiwa kukutana katika tamasha kubwa la sanaa na utalii la Arusha Arts and Craft Festival, linalolenga kuvumbua vipaji, kuunganisha wadau na kufungua fursa za ajira kwa vijana. Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 6 hadi 11 katika Viwanja vya General Tyre, likiwaleta pamoja wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi na Serikali. Akitangaza maandalizi ya tamasha hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tanzania International Tourism Festival, Ibrahim Othman Jama, ameeleza kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuleta tija ya kiuchumi na kijamii kupitia kuunganisha sanaa na utalii. “Tumekuja na mkakati wa mradi ambao unaweza kuunganisha Watanzania, kuwashauri, kuwaelekeza, lakini pia kuvumbua vipaji vyao.Mfumo huu utasaidia kutengeneza mustakabali wa vijana kupitia maendeleo, ajira na ubunifu (creativity) kwa maslahi mapana ya nchi yetu,” alisisitiza Jama. Jama aliongeza kuwa tamasha hilo linalenga pia kujenga kanzidata (database) kamili ya wasanii na wadau wa kazi za mikono na sanaa za ufundi, wakiwemo waliosajiliwa na wale ambao hawajasajiliwa, ili kurahisisha usimamizi na ushirikishwaji wao katika fursa mbalimbali za kimaendeleo. Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Edward Buganga alisema Baraza hilo limejipanga kikamilifu kuunga mkono juhudi za wadau binafsi katika kuinua sanaa za ufundi nchini. Buganga alibainisha kuwa, tofauti na matamasha mengi yaliyozoeleka ya muziki na fani nyingine, tamasha hili linakuja na mtazamo wa pekee wa kukuza sanaa za ufundi katika kiwango cha kimataifa. Pia alibainisha kuwa kufanyika kwa tamasha hilo mjini Arusha kunatoa fursa ya kipekee kwa wageni wa kimataifa na wajumbe wa Mkutano Mkubwa wa Mabunge Duniani unaotarajiwa kufanyika nchini kujionea utajiri wa utamaduni na sanaa ya Mtanzania. Ushirikiano huu kati ya Tanzania International Tourism Festival, BASATA, Bodi ya Filamu pamoja na Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) unadhihirisha azma ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuweka mazingira wezeshi kwa wasanii na kuendeleza uchumi wa ubunifu nchini.- Naye Mwakilishi kutoka Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Grace Byabato, alisema taasisi hiyo itashiriki kikamilifu kutoa elimu kwa wabunifu kuhusu namna ya kulinda kazi zao na kunufaika na mfumo wa mauzo endelevu badala ya kutegemea mauzo ya mara moja pekee. Mwakilishi wa Bodi ya Filamu Tanzania, Bope Kiungu, alieleza kuwa Bodi hiyo itaonyesha filamu mbalimbali kila siku viwanjani hapo, kuendesha mijadala ya kielimu na burudani, pamoja na kutoa huduma na fursa mbalimbali za sekta ya filamu na michezo ya kuigiza.
Tue, 22 Sep 2026 14:21:48 +0000ASILIMIA KUBWA YA WANAWAKE WANASHIRIKI KILIMO, UFUGAJI - WAZIRI MKUU
-Asema uwekezaji ni lazima ili Afya Moja ifanikiwe katika ngazi ya jamii WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema takribani theluthi mbili ya wanawake walioajiriwa katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwemo, hufanya kazi kwenye mifumo ya chakula na kilimo. “FAO inakadiria kuwa wanawake wanaunda zaidi ya asilimia 42 ya nguvu kazi katika mifumo ya chakula na kilimo duniani. Takwimu hizi zinaonyesha kwamba wanawake hawako pembezoni mwa mifumo ya chakula na kilimo; bali wako katika kiini cha mifumo hiyo,” amesema. Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Septemba 21, 2026) wakati akishiriki jopo la viongozi wa juu lililojadili Mwaka wa Kimataifa wa Mwanamke Mkulima – Mtazamo wa Afya Moja, lililofanyika katika Kituo cha Sheikh Zayed, Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma, Italia. Waziri Mkuu ambaye anashikiri Mkutano wa Kimataifa wa Kujadili Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema yeye mwenyewe anatoka katika jamii ambako sehemu kubwa ya shughuli za uzalishaji, hasa za kilimo na ufugaji, hufanywa na wanawake. “Katika jamii zetu nyingi, shughuli hizi mbili za kiuchumi zinaongozwa na wanawake, lakini mchango wao bado unakabiliwa na vikwazo, ikiwemo ukosefu wa fursa sawa ya kupata ardhi, fedha, teknolojia, huduma za ugani, masoko na kushiriki katika kufanya maamuzi,” alisema wakati akitoa mada yake kwenye jopo hilo llililowashirikisha mawaziri wa Kilimo, Chakula na Uvuvi kutoka Ufaransa na Ireland na kuongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Godfrey Magwenzi. Akifafanua zaidi, Dkt. Mwigulu alisema: “FAO inakadiria kwamba hata pale wanawake wanaposimamia mashamba yenye ukubwa sawa na yale yanayosimamiwa na wanaume, tofauti ya uzalishaji kwa kila eneo la ardhi kati ya wanawake na wanaume ni takribani asilimia 24. Wanawake wanaofanya kazi katika ajira zenye malipo ndani ya mifumo ya chakula na kilimo hupata, kwa wastani, asilimia 78 ya kipato kinachopatikana kwa kila dola anayopata mwanaume.” “Hizi si takwimu tu zinazoonyesha ukosefu wa usawa; zinawakilisha pia uzalishaji unaopotea, kipato kinachopotea na fursa zinazopotea za kujenga mifumo imara na yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za chakula. Na hapo ndipo dhana ya Afya Moja inapopata umuhimu mkubwa,” alisisitiza. Alisema mwanamke mkulima haoni afya ya binadamu, ya wanyama, ya mimea na ya mazingira kama sekta zinazojitegemea kwa kuwa analima chakula kwa ajili ya familia na jamii, anafuga mifugo, anasimamia maji na ardhi, anahifadhi na kusindika chakula, anafanya maamuzi kuhusu afya ya wanyama na lishe ya familia, na anakabiliana na ukame, mafuriko, wadudu na magonjwa. “Kwa hiyo, maamuzi yake yanaweza kuathiri lishe, usalama wa chakula, kinga dhidi ya magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, matumizi sahihi ya dawa za kuua vimelea, bioanuwai na uendelevu wa mazingira.” “Kumwezesha mwanamke ni kuwekeza si katika kilimo pekee, bali pia katika Afya Moja. Ikiwa tunataka Afya Moja ifanikiwe katika ngazi ya jamii, ni lazima tuwekeze kwa wanawake ambao tayari wanaitekeleza katika maisha yao ya kila siku,” alisisitiza. Akishiriki mjadala huo, Waziri wa Kilimo na Chakula wa Ufaransa, Bi. Annie Genevard alisema licha ya kuwa Ufaransa ni nchi inayohamasisha usawa kati ya wanaume na wanawake, bado kuna mazingira ambayo wanawake wanahisi kutoonekana. “Robo ya mameneja wa mashamba nchini Ufaransa ni wanawake. Si jambo la kushangaza kusikia mwakilishi wa mauzo (sales representative) anapofika shambani na kumuuliza mwanamke anayemkuta: “Ningependa kumuona bosi wa hili shamba.” Nao hujibu: “Mimi ndiye bosi.” Amekiri kuwa, bado kuna safari ndefu ya kufikia usawa na kwamba hawawezi kujenga mifumo ya kilimo na chakula yenye ustahimilivu zaidi bila kuchukua hatua kwa wakati mmoja kupunguza ukosefu huo wa usawa. Alisema alipoteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, aliamua kuanzisha mpango wa kuwainua wanawake kupitia mafunzo na kuongeza muonekano wao wa umiliki kwenye jamii yao. Lengo lake ni kuwasaidia zaidi wanawake wakulima katika maisha yao ya kila siku ili wapate taarifa bora kuhusu haki zao, hususan kuhusu uzazi, kuboresha huduma za kuchukua nafasi ya mkulima na kuboresha zaidi zana za kilimo ili ziendane na mahitaji yao. “Na niseme wazi hapa kuwa hatuko katika hatua ya kutoa ahadi pekee; tayari tumeanza kuchukua hatua. Tumeanza kuwatambua wanawake katika kilimo na pia kuwawezesha kutambuliwa kama wakulima kamili. Zaidi ya hayo, tumehakikisha mpango huu unaweza kupimwa na kufuatiliwa kwa muda. Kila hatua ina viashiria vya ufuatiliaji na matokeo.” Naye, Waziri wa Kilimo, Chakula na Masuala ya Uvuvi wa Ireland, Martin Heydon aliwaeleza washiriki wa jopo hili kwamba kabla hajawa Waziri wa Kilimo, alikuwa mkulima katika shamba alilorithi kutoka kwa mama yake. “Mimi na mke wangu bado tunaendesha shughuli za kilimo pamoja na watoto wetu wanne katika shamba letu. Shamba hilo nilirithi kutoka kwa mama yangu, kwa sababu baba yangu alifariki nilipokuwa na umri wa miaka minane tu,” alisema. “Mwaka 1986 wakati baba anafariki, mama yangu alikuwa na miaka 43. Alikuwa mama na baba yetu kwa wakati mmoja. Wakati mwingine alikuwa mwalimu wetu, muuguzi wetu, lakini daima alikuwa mkulima. Alisisitiza kuendelea na shughuli za kilimo wakati akitulea. Alitaka kutujengea upendo, shauku na maarifa kuhusu uzalishaji wa chakula, kutunza wanyama, kutunza ardhi na mambo mengine yanayohusiana na kilimo.” Alisema kuwa, kwa uzoefu wa Ireland, wanawake wakulima, madaktari wa mifugo wanawake, wanasayansi wanawake wa kilimo na watafiti wanawake wa mimea wako katika kiini cha maeneo yote hayo lakini mara nyingi mchango wao hautambuliwi kwa kiwango kinachostahili. “Wanawake bado ndiyo walezi wakuu katika kaya nyingi za vijijini nchini Ireland, wakishiriki katika kupanga lishe ya familia, usalama wa chakula nyumbani na kubeba mzigo wa kiafya pale kipato cha shamba kinapokuwa hakina uhakika au majukumu yanapokutana na kazi za nje ya shamba. Mkakati wowote makini wa Afya Moja lazima uzingatie kazi hii isiyolipwa na ambayo kwa kiasi kikubwa haionekani kama sehemu ya mfumo huo,” alisema. Alisema kizazi kipya nchini humo kinahusiana na maeneo yote hayo lakini kuna wakulima wachache sana ambao wana umri chini ya miaka 35. “Urithi wa mashamba nchini Ireland kwa muda mrefu umekuwa ukifuata utamaduni wa kumrithisha mwanaume. Tume yetu huru kuhusu kizazi kipya katika kilimo iliweka wazi kwamba kusaidia urithi wa mashamba na kuboresha usawa wa kijinsia ni jukumu moja, si mambo mawili tofauti. Binti yangu mwenye umri wa miaka mitano, ana nafasi sawa kabisa ya kurithi shamba letu kama ndugu zake watatu wa kiume,” alisisitiza. Waziri huyo alisema anaamini kwamba ili kuwa na uendelevu wa kweli katika nyanja za kiuchumi, kimazingira na kijamii, ni lazima kuhakikisha wanawake wanakuwa na nafasi sawa na wanaume katika mifumo ya chakula na kilimo. Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu amefuatana na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi na watendaji wengine wa Serikali.
Tue, 22 Sep 2026 14:29:26 +0000SERIKALI YASISITIZA UMUHIMU WA KULINDA MAZINGIRA NA RASILIMALI ZA BAHARI
Na Oscar Assenga, TANGA SERIKALI imesisitiza umuhimu wa kulinda mazingira na rasilimali za bahari, ikisema uharibifu wake unaweza kuhatarisha maisha ya wananchi, miundombinu na shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazotegemea bahari, mito na maziwa. Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar (SMZ), Mhandisi Ally Saidi Bakari, aliyemwakilisha Waziri wa Uchukuzi wa Zanzibar wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Usafiri Majini Duniani yaliyofanyika mkoani Tanga. Mhandisi Ally amesema Tanzania ina utajiri mkubwa wa rasilimali za maji, ikiwemo bahari, mito na maziwa, ambazo zimekuwa nguzo muhimu ya ajira na kipato kwa wananchi kupitia uvuvi, utalii, biashara, usafirishaji, kilimo cha mwani na shughuli nyingine za uchumi wa bluu Hata hivyo, amesema rasilimali hizo zinakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uharibifu wa mifumo ya ikolojia, mabadiliko ya tabianchi na matumizi yasiyozingatia uendelevu. Amesema hali hiyo inahitaji ushirikiano wa Serikali, wananchi na wadau katika kuhakikisha mazingira ya bahari yanalindwa ili yaendelee kuwa chanzo cha fursa na maendeleo kwa vizazi vya sasa na vijavyo. “Maji ni uhai, yawe baharini, mitoni au maziwa. Tusipoyaheshimu maji yatatushughulikia. Nguvu ya maji ni kubwa sana na tunapaswa kutambua umuhimu wake na kulinda rasilimali zilizopo,” amesema. Ameonya kuwa uharibifu wa mazingira ya bahari unaweza kusababisha madhara makubwa, yakiwemo kupotea kwa rasilimali, kuathiri maisha ya wananchi na kuharibu miundombinu pamoja na makazi ya watu wanaoishi katika maeneo ya mwambao. Kwa mujibu wa Mhandisi Ally, Tanzania inapaswa kutumia fursa zinazotokana na kuwa na bahari, mito na maziwa katika kukuza uchumi, huku ikiweka mkazo katika uhifadhi wa mazingira na usalama wa shughuli za usafirishaji majini. Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya bandari na usafirishaji wa majini, akiwapongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi za kuboresha miundombinu hiyo. Ametaja maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Zanzibar na Bandari ya Tanga, pamoja na miundombinu ya usafirishaji katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, kuwa sehemu ya hatua zinazolenga kuongeza matumizi ya rasilimali za maji katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Aidha, amesema usalama wa vyombo vya usafiri majini unapaswa kupewa kipaumbele kutokana na kuwepo kwa ajali katika bahari, mito na maziwa. Ametaka taasisi zinazohusika kuendelea kufanya ukaguzi wa vyombo vya usafiri majini kabla na wakati vinapotumika ili kupunguza ajali na kulinda maisha ya abiria pamoja na mali zao. Amesema maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yanatoa fursa kwa Serikali, wadau na wananchi kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya bahari na kutafuta suluhisho, ikiwemo namna ya kupunguza ajali za majini na kulinda mazingira. TANGA Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Rashid Mchatta, amesema kuchaguliwa kwa Tanga kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kunatokana na fursa nyingi za kiuchumi zinazopatikana kutokana na jiografia ya mkoa huo wenye mwambao wa bahari. Mchatta amesema Tanga inaendelea kuwa kitovu cha shughuli za uchumi wa bluu, ikiwemo uvuvi, utalii, biashara na shughuli nyingine zinazohusiana na matumizi ya rasilimali za bahari. Amesema maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Tanga yamechangia kuongeza shughuli za kiuchumi katika mkoa huo, akibainisha kuwa idadi ya meli zinazofika bandarini hapo imeongezeka hadi takribani meli 17 kwa mwezi, kutoka meli moja kwa mwezi katika kipindi cha nyuma. Amesema ongezeko hilo limefungua fursa zaidi za biashara na shughuli nyingine zinazozunguka bandari, huku akitaja pia miradi ya kimkakati ikiwemo bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga, kuwa miongoni mwa shughuli zinazoongeza umuhimu wa Mkoa wa Tanga katika uchumi wa nchi. Hata hivyo, Mchatta amesema ongezeko la shughuli za bandari na uwekezaji linapaswa kwenda sambamba na ulinzi wa mazingira ya bahari ili kuhakikisha fursa hizo zinaendelea kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu. Maadhimisho ya Siku ya Usafiri wa Majini Duniani yanatoa nafasi ya kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa usafiri wa majini, usalama wa vyombo na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari. Kwa Tanzania, yenye bahari, mito na maziwa, rasilimali hizo zinaendelea kuwa muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii, jambo linaloifanya hifadhi na matumizi endelevu kuwa msingi wa kuhakikisha zinaendelea kuwa chanzo cha ajira, kipato na maendeleo.
Tue, 22 Sep 2026 14:31:04 +0000MAKAMU WA RAIS AWASILI NEW YORK KUMWAKILISHA RAIS SAMIA UNGA81
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratias Ndejembi, amewasili jijini New York, Marekani, kwa ajili ya kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA81). Mhe. Ndejembi amewasili nchini Marekani kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa John F. Kennedy, ambapo amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Elsie Kanza, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York, Mhe. Togolani Mavura, pamoja na maafisa mbalimbali. Mkutano huo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unawakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na viongozi mbalimbali kutoka mataifa duniani kujadili masuala muhimu ya kimataifa, yakiwemo uchumi, siasa, mazingira na haki za binadamu. Mkutano wa mwaka huu unaongozwa na kaulimbiu “Kurudisha Imani, Kusimamia Mabadiliko: Umoja wa Mataifa Unaohudumia Wote” (Restoring Trust, Managing Transformation: A United Nations That Delivers for All). Kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza kujenga upya uaminifu na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na mabadiliko makubwa yanayoendelea duniani, ikiwemo maendeleo ya kasi ya teknolojia ya akili unde (AI). Katika ziara hiyo, Mhe. Ndejembi anatarajiwa kuhutubia Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kushiriki katika shughuli mbalimbali za mkutano huo, zikiwemo Mjadala Mkuu (General Debate), mikutano ya pembezoni pamoja na mikutano ya pande mbili (Bilateral Meetings) na viongozi na wawakilishi wa mataifa mbalimbali.
Tue, 22 Sep 2026 14:41:11 +0000DEREVA TARURA AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUMTISHIA DEREVA WA BASI KWA TOYI YA BASTOLA
Na Janeth Raphael – MichuziTv Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linamshikilia dereva wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Dodoma, Sath John Masawa (31), kwa tuhuma za kumtishia dereva wa basi la SATCO kwa kutumia kitu kinachodhaniwa kuwa bastola, kufuatia tukio la mgongano wa magari lililodaiwa kutokea jijini Dodoma. Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, tukio hilo lilihusisha basi la SATCO aina ya Yutong, lenye namba za usajili T 308 EME , lililokuwa likiendeshwa na Said Fadhili (54), ambaye alidaiwa kukwanguliwa na gari aina ya Land Cruiser LX 70 Series linalomilikiwa na TARURA, wakati akitoka kuweka mafuta katika kituo cha TotalEnergies. Baada ya tukio hilo, inadaiwa kuwa dereva wa gari hilo la TARURA, Sath John, alimtishia Said kwa kutumia kitu kilichodhaniwa kuwa bastola, hali iliyosababisha tukio hilo kuripotiwa katika Jeshi la Polisi. Polisi walifika eneo la tukio na kumkamata Sath John. Baada ya kumfanyia upekuzi, ilibainika kuwa kitu alichokuwa amevaa kiunoni hakikuwa bastola halisi, bali ni toyi iliyotengenezwa kwa kufanana na bastola . Katika uchunguzi wa awali, Jeshi la Polisi pia lilibaini kuwa gari la TARURA lililohusika katika tukio hilo, ambalo namba zake halali ni STM 5806 , lilikuwa likitumia namba za usajili T 881 ENZ wakati wa tukio. Kwa mujibu wa Polisi, namba hiyo inadaiwa kuwa ya gari jingine linalomilikiwa na mtu mwingine. Jeshi la Polisi linaendelea kumshikilia Sath John kwa ajili ya mahojiano na kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo kabla ya hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa. Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limewataka madereva kuacha kutumia namba za usajili zisizo halali kwenye magari, likieleza kuwa matumizi ya namba hizo yanaweza kuficha utambulisho halisi wa gari na ni kinyume cha sheria.
Tue, 22 Sep 2026 15:15:47 +0000RABIA ASISITIZA UMOJA, AMANI NA MSHIKAMANO
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Ndg. Rabia Abdalla Hamid (MCC) , amesisitiza umuhimu wa kila mwananchi kutimiza wajibu wake katika kudumisha umoja, mshikamano, amani na utulivu nchini. Ndg. Rabia ameyasema hayo leo Septemba 22, 2026, baada ya kupokelewa katika Ofisi za CCM Mkoa wa Morogoro, ambapo ametembelea vikundi vya wajasiriamali na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi, huku baadhi ya changamoto hizo zikitatuliwa papo hapo. Aidha, Ndugu Rabia ametumia nafasi hiyo kuzungumza na makundi mbalimbali ya kijamii, akisisitiza kuwa amani, umoja na mshikamano ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi. Amesema kila mwananchi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana wajibu wa kulinda na kudumisha amani, utulivu, umoja na mshikamano kwa maslahi ya Watanzania wote. Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na taasisi mbalimbali katika kutatua changamoto zinazowakabili na kujenga jamii yenye mshikamano na mazingira rafiki kwa maendeleo.
Tue, 22 Sep 2026 15:34:53 +0000WAZIRI AWESO AKATAA NYONGEZA YA MUDA MRADI WA MAJI WA BILIONI 53.12 TANGA
Na Oscar Assenga, TANGA WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa hati fungani wenye thamani ya Sh bilioni 53.12 kuongeza nguvu kazi na kuhakikisha unakamilika ifikapo Novemba 30, mwaka huu, akisisitiza kuwa hakuna muda wa nyongeza utakaotolewa. Aweso ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, ikiwamo tanki kubwa la maji lililopo Mowe jijini Tanga, ambapo alisema serikali haitakuwa tayari kusikia visingizio kutokana na fedha za utekelezaji wa mradi huo kuwepo. Alisema hadi sasa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 70 ya utekelezaji, hivyo mkandarasi anatakiwa kuongeza kasi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha wananchi wanaanza kunufaika na huduma hiyo kwa wakati uliopangwa. “Nimekuja leo kukagua huu mradi nikiwa na Katibu Mkuu. Mradi huu sasa umefikia asilimia 75. Maelekezo ambayo nawaambia Tanga Uwasa na mkandarasi ni kwamba hatutakuwa na muda wa nyongeza. “Utendaji wa mradi huu unatakiwa kubadilika kuanzia sasa. Mradi huu una fedha, hakuna kisingizio. Ni suala la mkandarasi kuongeza watu kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati,” alisema Aweso. Aliongeza: “Utendaji ubadilike. Mkandarasi anatakiwa kufanya kazi usiku na mchana. Tunataka mwisho wa mwezi huu wa 10 tukija kuona maendeleo yake, yatupatie picha kwamba ifikapo Novemba 30, 2026, mradi utakuwa umekamilika. “Hatuna kisingizio kwa sababu fedha zipo, na fedha hizi ni zile ambazo wananchi wameweza kujitolea kuchangia taasisi hii ya Tanga Uwasa.” Aweso alisema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya mfano katika Wizara ya Maji inayotekelezwa kwa kutumia hati fungani kama chanzo mbadala cha fedha kwa ajili ya kuimarisha huduma ya maji. Alisema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na chanzo cha uhakika cha maji kitakachosaidia wananchi kupata huduma hata pale linapotokea tatizo la kiufundi au kukatika kwa umeme. Kwa mujibu wa Aweso, hatua hiyo pia inaendana na agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutaka taasisi za umma kuwa na vyanzo mbadala vya fedha ili kuongeza uwezo wa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, alisema wizara hiyo itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga Uwasa) katika kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba. Alisema timu ya wizara itafuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Aweso, akisisitiza kuwa ifikapo Novemba 30, 2026, miundombinu yote inayohusika na mradi inapaswa kuwa imekamilika na wananchi kuanza kupata huduma. TANGA UWASA Mkurugenzi wa Tanga Uwasa, Geoffrey Hilly, alisema mradi huo unaendelea vizuri na kwa sasa umefikia wastani wa asilimia 72 kwa ujumla, ikiwamo kazi zinazotekelezwa na wakandarasi katika maeneo mbalimbali kuanzia chanzo hadi usambazaji wa mabomba mitaani. Alisema mradi huo unalenga kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Tanga pamoja na Wilaya za Muheza na Mkinga, huku Mkinga ikiwa miongoni mwa maeneo yatakayonufaika zaidi na maji yanayozalishwa katika mtambo wa Mowe. Kwa mujibu wa Hilly, mradi huo unahusisha upanuzi wa mtambo wa uzalishaji maji kutoka uwezo wa kuzalisha lita milioni 45 hadi lita milioni 60 kwa siku. Alisema pia unahusisha ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita milioni 35, litakalosaidia kuhakikisha maji yanapatikana hata katika vipindi vya changamoto za kiufundi. Alisema tanki hilo lina uwezo wa kuhifadhi maji ya kutosha kwa matumizi ya takribani saa 18, hatua inayotarajiwa kusaidia wananchi kupata huduma ya maji kwa uhakika zaidi kwa saa 24. MKANDARASI Meneja wa mradi huo kutoka kampuni ya China Railway Seventh Group, Dai Bin, aliahidi kuongeza nguvu kazi na kuhakikisha utekelezaji unakwenda kwa kasi ili kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliowekwa. Dai alisema kampuni hiyo imepokea maelekezo ya Waziri Aweso na kwamba itaongeza muda wa kazi kwa kufanya shughuli za ujenzi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Tue, 22 Sep 2026 15:36:27 +0000MAKAMU WA RAIS KUHUTUBIA KIKAO CHA 81 CHA BARAZA KUU LA UMOJA WA MATAIFA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi leo Jumanne, Septemba 22, 2026, anatarajiwa kuhutubia Mjadala Mkuu wa Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 81), unaofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. Makamu wa Rais anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika mkutano huo wa ngazi ya juu unaowakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali, pamoja na wawakilishi wa ngazi za juu kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Mjadala Mkuu wa mwaka 2026 unafanyika chini ya kaulimbiu, “Kurejesha imani, kusimamia mabadiliko: Umoja wa Mataifa unaowatumikia wote” (Restoring trust, managing transformation: A United Nations that delivers for all). Miongoni mwa mambo yanayojadiliwa katika mkutano huo ni changamoto mbalimbali zinazoikabili Dunia na namna ya kuimarisha ushirikiano katika kutafuta suluhisho la kudumu, hususan katika masuala ya amani na usalama wa kimataifa, maendeleo endelevu, mabadiliko ya tabianchi, afya, utawala wa teknolojia na Matumizi ya akili unde (AI), pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kupitia Umoja wa Mataifa. Mjadala Mkuu wa Kikao cha 81 umeanza leo, Septemba 22, na utaendelea hadi Septemba 26, kabla ya kuhitimishwa Septemba 28, 2026.
Tue, 22 Sep 2026 17:33:48 +0000TAEC YAFICHUA MAPUNGUFU YA USALAMA WA MIONZI KATIKA VITUO 16 PWANI
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeendelea kuimarisha usimamizi wa usalama wa mionzi nchini kupitia operesheni ya ukaguzi wa vituo vinavyotumia vifaa na vyanzo vya mionzi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kuhakikisha matumizi ya mionzi yanafanyika kwa usalama. Operesheni hiyo inayotekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Nguvu za Atomu Na. 7 ya mwaka 2003, inalenga kuhakikisha vituo vinavyotoa huduma zinazohusisha matumizi ya mionzi vinakuwa na leseni halali, wataalamu wenye sifa zinazotakiwa pamoja na vifaa vilivyo katika hali nzuri na vinavyokidhi viwango vya usalama. Katika Mkoa wa Pwani, TAEC ilifanya ukaguzi kuanzia Septemba 2 hadi 16, 2026, ambapo timu ya wataalamu wa Tume ilitembea umbali wa takribani kilomita 1,450 katika maeneo ya Kibaha, Bagamoyo, Kisarawe, Kibiti, Rufiji, Mkuranga na Mafia. Jumla ya vituo 35 vilikaguliwa katika mkoa huo, vikiwemo hospitali, vituo vya afya na kliniki, pamoja na maeneo mengine yanayotumia vifaa au vyanzo vya mionzi, ikiwemo viwanda na maeneo yenye mifumo ya ukaguzi wa mizigo. Matokeo ya ukaguzi huo yanaonesha kuwa vituo 19 kati ya 35 vilivyokaguliwa vilikidhi mahitaji muhimu ya usalama wa mionzi na kuwa na leseni halali. Vituo 16 vilibainika kuwa na mapungufu mbalimbali yanayohitaji kufanyiwa marekebisho ili kukidhi matakwa ya sheria na viwango vya usalama. Miongoni mwa mapungufu yaliyobainika ni baadhi ya vituo kutoa huduma bila kuwa na leseni halali, kutokidhi baadhi ya masharti ya usalama, kuwa na mashine zinazohitaji matengenezo pamoja na kukosekana kwa wataalamu wenye sifa zinazotakiwa. Baadhi ya vituo pia havikuwa vikitoa huduma zinazohusisha matumizi ya mionzi wakati ukaguzi ulipofanyika. Akizungumzia ukaguzi huo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TAEC, Peter Ngamilo, amesema hatua hiyo ni sehemu ya majukumu ya Tume ya kuhakikisha matumizi ya mionzi nchini yanafanyika kwa usalama kwa wagonjwa, watumishi na wananchi kwa ujumla. “Tunafanya ukaguzi huu kuhakikisha huduma zinazohusisha matumizi ya mionzi zinatolewa kwa kuzingatia usalama wa mgonjwa, mtoa huduma na wananchi. Katika Mkoa wa Pwani, vituo 19 kati ya 35 vilivyokaguliwa vimekidhi mahitaji muhimu, huku vituo 16 vikibainika kuwa na mapungufu yanayopaswa kurekebishwa,” amesema Ngamilo. Amesema TAEC itaendelea kuvifuatilia vituo vilivyobainika kuwa na mapungufu na kutoa maelekezo ya kitaalamu ili viweze kurekebisha kasoro hizo na kukidhi matakwa ya sheria. Ngamilo ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa ukaguzi katika Mkoa wa Pwani, TAEC imeendelea na operesheni hiyo katika maeneo mengine nchini, ambapo vituo 32 vimekaguliwa katika Mkoa wa Lindi na vituo 40 Zanzibar. Hivyo, jumla ya vituo 107 vimekaguliwa katika Pwani, Lindi na Zanzibar. Amesema ukaguzi pia umefanyika katika Mkoa wa Njombe na taarifa zake zinaendelea kuchakatwa, huku operesheni hiyo ikiendelea hivi sasa katika Mkoa wa Morogoro. Amesisitiza kuwa dhamira ya TAEC katika ukaguzi huo ni kuhakikisha sheria na taratibu za usalama wa mionzi zinazingatiwa, sambamba na kutoa elimu na maelekezo ya kitaalamu kwa wamiliki na waendeshaji wa vituo vinavyotumia vifaa na vyanzo vya mionzi. “Tunatoa wito kwa wamiliki na waendeshaji wa vituo vinavyotumia vifaa au vyanzo vya mionzi kuhakikisha wana leseni halali, vifaa vyao vinakidhi viwango na wana wataalamu wenye sifa zinazotakiwa. TAEC itaendelea kufanya ukaguzi na kutoa elimu ili kuhakikisha matumizi ya mionzi nchini yanafanyika kwa usalama,” amesema Ngamilo. Ameongeza kuwa usimamizi madhubuti wa matumizi ya mionzi ni muhimu katika kulinda afya za wagonjwa, watumishi wanaofanya kazi katika mazingira yenye mionzi, wananchi pamoja na mazingira.
Tue, 22 Sep 2026 17:42:05 +0000KATA 11 NGORONGORO MWENDO MDUNDO RHINO CUP, BINGWA KUSHUHUDIA MTANANGE WA SIMBA NA YANGA
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imezindua mashindano bab kubwa ya mchezo wa mpira wa miguu yatakayojulikana Kama Rhino Cup kutoa hamasa kwa jamii ya tarafa ya Ngorongoro yenye vijiji 25 na Kata 11 kutoshana nguvu katika mchezo wa kabumbu. Mashindano hayo yamefunguliwa jumanne hii katika viwanja vya shule ya msingi Makao Ngorongoro na kocha wa zamani wa timu ya taifa (Taifa Stars ) na Yanga Charles Boniface Mkwasa. Akifungua mashindano hayo Mkwasa amewataka vijana wa tarafa ya Ngorongoro kutumia michezo Kama fursa ya ajira na kujenga afya zilizo bora na kuhimiza uhifadhi shirikishi kupitia michezo. Naibu kamishna wa Uhifadhi NCAA Aidan Makalla amesema Mamlaka imeamua kuanzisha kombe hilo litakalochezwa kila mwaka ili kutoa hamasa ya mchezo wa mpira wa miguu ndani ya tarafa ya Ngorongoro na kuhamasisha jamii juu ya ulinzi wa faru na rasilimali mbalimbali zilizopo ndani ya hifadhi. Mashindano hayo yatashirikisha kata 11 za tarafa ya Ngorongoro na bingwa wa mashindano hayo pamoja na zawadi nyingine ataenda kushuhudia mtanange wa ligi kuu baina ya Simba na Yanga kwa msimu wa mwaka huu.
Tue, 22 Sep 2026 19:14:21 +0000MWENYEKITI (UVCCM) GEITA AICHOTA TEKNOLOJIA YA MABASI KUKUZA USAFIRISHAJI CHINA
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Geita, Manjale Magambo, ametembelea kiwanda kikubwa cha kutengeneza mabasi cha Yutong kilichopo Zhengzhou nchini China kwa mwaliko rasmi. Ziara hiyo inalenga kujifunza teknolojia na mbinu za kisasa zinazotumika katika sekta ya usafirishaji ili kuona namna zinavyoweza kusaidia kukuza uchumi na kufungua fursa kwa vijana nchini. Akiwa kiwandani hapo, Magambo alipata fursa ya kujionea kwa vitendo mchakato mzima wa uzalishaji wa mabasi, kuanzia usanifu hadi hatua za mwisho, jambo lililompa uelewa wa karibu kuhusu teknolojia na mifumo bora inayotumika Akizungumza baada ya ziara hiyo, Magambo alisema China imefanikiwa kuitumia sekta ya usafirishaji kama injini muhimu ya maendeleo ya uchumi kwa kuunganisha teknolojia na ufanisi. “Ziara hii imetupa nafasi ya kujifunza na kuona kwa vitendo namna teknolojia inavyotumika katika sekta ya usafirishaji. Tumepata uzoefu ambao tunaweza kuutumia katika kutafakari fursa mbalimbali za maendeleo na kuwawezesha vijana kushiriki zaidi katika uchumi,” alisema Magambo. Aliongeza kuwa uzoefu aliopata ni muhimu kwa vijana wa Kitanzania kufahamu fursa zilizopo katika sekta ya usafirishaji, zikiwemo uwekezaji, ajira na ujasiriamali. Kwa mujibu wake, vijana wanapaswa kuwa tayari kujifunza teknolojia na mifumo mipya ya uzalishaji kutoka sehemu mbalimbali duniani kwani dunia inabadilika kwa kasi na teknolojia imekuwa nguzo ya maendeleo. Magambo alisisitiza kuwa maarifa hayo hayapaswi kuishia kwenye ziara pekee, bali yanapaswa kutumika kujenga mawazo mapya yatakayosaidia kuongeza ajira na shughuli za kiuchumi kwa vijana na wananchi kwa ujumla.
Tue, 22 Sep 2026 19:27:44 +0000Jumuiya ya Madola Yapongeza Hatua za Maridhiano Tanzania
Kamati ya Mawaziri cha Jumuiya ya Madola wanaosimamia Utekelezaji wa Maadili (CMAG) imetambua na kufurahishwa na ushirikiano mzuri ulioonyeshwa na serikali ya Tanzania pamoja na hatua zilizochukuliwa kuwezesha maridhiano huko Zanzibar. Kamati hiyo katika kikao chake cha 74 imesema hatua hizo zilizochukuliwa ni msingi thabiti wa maendeleo zaidi ya kidemokrasia na kisiasa nchini Tanzania. Kikao hicho maalum kiliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ulaya wa Malta, Mheshimiwa Chris Fearne. Katika kikao hicho kilichofanyika mjini New York, viongozi na wawakilishi mbalimbali wa ngazi za juu walihudhuria, wakiwemo Naibu Waziri Mkuu wa Samoa, Mheshimiwa Mulipola Anarosa Ale Molioʻo, pamoja na mawaziri na wawakilishi maalum kutoka nchi wanachama wa Antigua na Barbuda, Botswana, Canada, Grenada, Malaysia, Mauritius, na Zambia. Uwepo wa viongozi hawa ulitoa fursa ya kufanya tathmini ya kina kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu nchi wanachama, ikiwemo Tanzania na Uganda, na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora, na ushirikiano ndani ya familia ya Jumuiya ya Madola. Katika taarifa iliyotolewa kufuatia kikao chao maalum kilichofanyika pembezoni mwa Mkuu wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York, pamoja na kutambua maendeleo hayo chanya katika maeneo mbalimbali, CMAG ilisisitiza haja ya kuendelea kufanya kazi ya ziada ili kuhakikisha kunakuwa na mchakato jumuishi na wa wazi wa mazungumzo ya kisiasa ya vyama vingi, sambamba na kulinda kwa dhati uhuru wa kiraia, kisiasa, na vyombo vya habari. Kabla ya taarifa kamati hiyo ili ilipokea taarifa iliyowasilishwa kwa kina na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Prof. Palamagamba Kabudi. CMAG imesifu utayari wa nchi ya Tanzania kushirikiana na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo katika kuimarisha misingi ya maridhiano na maelewano ya kitaifa. Hata hivyo walitilia mkazo maalum katika umuhimu wa kuzingatia taratibu za kisheria zilizo wazi, za haki na kwa wakati unaofaa katika mashauri yote yaliyopo wazi, pamoja na kuweka michakato inayoaminika ya uwajibikaji, utoaji wa haki na fidia stahiki kwa wale wote waliothiriwa na matukio mbalimbali ya nyuma, ili kuimarisha zaidi uaminifu na ustawi wa jamii. Kufuatia tathmini hiyo ya kina, Jumuiya ya Madola imeihimiza serikali ya Tanzania kupanga tarehe ya mapema kwa ajili ya ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ili apate fursa ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na wadau wengine muhimu wa maendeleo na siasa nchini. Kutokana na umuhimu wa mazungumzo hayo na hatua zinazoendelea kuchukuliwa, kikao hicho kiliafikia makubaliano ya kuendelea kuweka Tanzania kwenye ajenda yake rasmi ya ufuatiliaji, huku wakithibitisha utayari wa kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu na serikali katika kuhakikisha malengo ya kidemokrasia, amani, na maendeleo endelevu yanatimizwa kwa maslahi mapana ya wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kamati hiyo ya Mawaziri cha Jumuiya ya Madola inayosimamia Utekelezaji wa Maadili (CMAG) ilianzishwa mwaka 1995 ili kuwa mlinzi na mtetezi wa maadili na misingi ya kisiasa ya Jumuiya ya Madola. Kamati hiyo inaundwa na mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi wanachama nane zinazozunguka kanda mbalimbali kwa mfumo wa zamu, ikijumuisha pia waziri wa mambo ya nje wa nchi iliyo Mwenyekiti Mkuu wa sasa wa Jumuiya hiyo ambaye ni mwenyeji wa Mkutano uliopita wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM). Kikao hicho cha 74 kiliitishwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Mheshimiwa Shirley Botchwey.
Tue, 22 Sep 2026 19:35:34 +0000Sitoyo Lopokoiyit underscores Absa's confidence in Tanzania's growth potential
Tanzania’s expanding economy and growing digital financial services sector have attracted renewed attention from Absa Group, which has reaffirmed its long-term commitment to the country. The Group’s Chief Executive for Personal and Private Banking Pan-Africa, Sitoyo Lopokoiyit, made the remarks during a visit to Tanzania, where he engaged customers, employees, business leaders and other stakeholders. The visit provided an opportunity to discuss customer needs, economic opportunities and the role of financial institutions in promoting inclusive growth. According to Mr Lopokoiyit, Tanzania’s economic momentum, expanding middle class and growing trade corridors were contributing to the country’s increasing importance in East Africa. “Tanzania is a market with tremendous potential and an increasingly important role in East Africa’s growth story,” he said. He said the changing financial needs of customers required banks to provide services that were accessible, convenient and responsive to their ambitions. “Whether they are growing a business, buying a home, investing for the future or making everyday transactions, our focus is on delivering solutions that are simple, accessible and relevant to their needs,” he said. Mr Lopokoiyit also pointed to digital transformation as a major opportunity for expanding financial access in Tanzania. He said the integration of technology, professional expertise and strong partnerships could help banks deliver more meaningful outcomes for customers. “As digital adoption continues to accelerate in Tanzania, we see significant opportunity to support customers with solutions that enable growth, inclusion and prosperity,” he said. Absa Bank Tanzania Managing Director Obedi Laiser said the Group’s continued interest in Tanzania reflected the country’s position within its broader African strategy. He said investment, trade expansion and digital adoption were creating opportunities that could benefit individuals, businesses and communities. “Tanzania is experiencing strong growth driven by increasing investment, expanding trade opportunities and rapid digital adoption, creating significant potential for individuals, businesses and communities to prosper,” Mr Laiser said. He said Absa Bank Tanzania would continue to strengthen its financial solutions, relationship banking services and digital capabilities in response to customer needs. The Managing Director added that the bank remained committed to supporting opportunities that contribute to sustainable economic growth and shared prosperity. Absa said its investments in digital platforms, payment solutions and customer experience were intended to improve access to banking services and help customers participate in economic opportunities both locally and across the continent. The Group’s pan-African network, it said, would continue to support connections between customers and markets as it strengthened its operations in Tanzania. The visit comes as Absa seeks to deepen its engagement with the Tanzanian market and reinforce its support for the country’s economic development.
Wed, 23 Sep 2026 04:00:00 +0000NYONGO AWATAKA WAFUGAJI KUACHA KUINGIZA MIFUGO MASHAMBANI
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo , amewaagiza wafugaji mkoani humo kuacha mara moja kuingiza na kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia uharibifu wa mazao unaosababishwa na mifugo. Nyongo alitoa agizo hilo Septemba 22, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri za Mji wa Rufiji na Kibiti, ambako alisikiliza kero za wananchi na kutoa maelekezo ya hatua za kuchukuliwa. Alisema Serikali haiwezi kuendelea kushuhudia mazao ya wakulima yakiharibiwa na mifugo, wakati maeneo yametengwa kwa ajili ya kilimo na ufugaji. “Hatukubali kuendelea kuona mazao ya wakulima yakiharibiwa wakati kila kundi limetengewa maeneo kwa ajili ya shughuli zake. Wafugaji waheshimu maeneo ya wakulima na waache mara moja kuingiza mifugo kwenye mashamba,” alisema. Aidha, alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Rufiji kusimamia utekelezaji wa agizo hilo na kuhakikisha wafugaji watakaobainika kuingiza au kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Katika hatua nyingine, Nyongo aliipongeza Halmashauri ya Rufiji kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuvuka malengo yaliyowekwa, huku akizitaka Halmashauri za Rufiji na Kibiti kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato ili kuongeza uwezo wa Serikali za mitaa kutoa huduma bora kwa wananchi. Kuhusu utabiri wa mvua kubwa za msimu wa Vuli unaohusishwa na hali ya El Niño , Nyongo alizitaka halmashauri hizo kuimarisha maandalizi na kuchukua hatua za tahadhari mapema ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza. Aliwataka wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni na maeneo mengine hatarishi kuhama mapema na kuhamia maeneo salama, akisisitiza kuwa usalama wa maisha ya wananchi unapaswa kupewa kipaumbele. Pia, aliwataka Wakuu wa Wilaya za Rufiji na Kibiti kutambua na kuainisha maeneo salama yatakayotumika kuwaweka wananchi watakaoweza kuathiriwa na mvua hizo, pamoja na kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana katika maeneo hayo. Ziara hiyo ni ya kwanza ya kikazi kwa Nyongo katika halmashauri hizo tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, ikiwa na lengo la kujitambulisha, kusikiliza kero za wananchi na kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Wed, 23 Sep 2026 06:28:24 +0000MUHIMBILI YAPOKEA MSAADA WA TZS. 23 MIL KUTOKA LIONS CLUB INTERNATIONAL
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), leo imepokea vifaa vya kutolea huduma za tiba aina ya Infusion Pumps vyenye thamani ya Shilingi milioni 23, vilivyotolewa na Lions Club International, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ubora wa huduma za afya na kuongeza usalama wa wagonjwa wakati wa matibabu. Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi, Dkt. Mbonea Yonazi, ameishukuru Lions Club International kwa mchango huo muhimu, na kuongeza kuwa vifaa hivyo vitaenda kuongeza ufanisi wa matibabu na usalama wa wagonjwa. “ Vifaa hivi vitasaidia kuboresha utoaji wa huduma na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma sahihi kulingana na mahitaji yao, huu ni mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa mgonjwa na ubora wa huduma tunazozitoa,”amesema Dkt. Yonazi. MNH inaendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa katika huduma za afya, hatua inayochangia kuongeza ufanisi, usahihi na usalama wa huduma kwa wagonjwa.
Wed, 23 Sep 2026 07:40:58 +0000TANZANIA YAPIGA HATUA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO, YAWANIA KITI BARAZA LA USALAMA UN
NEW YORK, Marekani TANZANIA imetangaza rasmi azma ya kuwania nafasi ya uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) kwa kipindi cha mwaka 2029–2030, ikiahidi kupeleka sauti imara ya Afrika na kusukuma mbele diplomasia ya kuzuia migogoro, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani na mageuzi ya operesheni za kulinda amani. Msimamo huo umetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mjadala wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika jijini New York, Marekani. Mhe. Ndejembi amesema iwapo Tanzania itachaguliwa, itatoa kipaumbele kwa diplomasia ya kuzuia migogoro kabla haijageuka kuwa vita, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani, kuimarisha nafasi ya wanawake katika ulinzi na ujenzi wa amani, kuongeza ushiriki wa vijana katika ajenda ya amani na usalama, pamoja na kusukuma mbele mageuzi ya operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani. Amesema azma hiyo imepata uungwaji mkono wa Umoja wa Afrika (AU), huku uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Usalama kwa kipindi hicho ukitarajiwa kufanyika Juni 2028. TANZANIA YASISITIZA MAGEUZI UN Katika hotuba hiyo, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuendelea kufanyika kwa mageuzi katika Umoja wa Mataifa ili kuimarisha misingi ya haki, usawa na uwakilishi wenye uwiano, badala ya mfumo wa kimataifa kuendelea kuakisi zaidi nguvu na ushawishi wa mataifa machache. Mhe. Ndejembi amesema mageuzi hayo ni muhimu zaidi katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na migogoro na vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa, kasi ya maendeleo ya Akili Mnemba (AI) na changamoto za usalama wa nishati. TANZANIA YAPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO Akizungumzia afya ya mama na mtoto, Mhe. Ndejembi amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya mama na mtoto, ikiwamo kuongeza kiwango cha uzazi unaofanyika katika vituo vya afya kutoka asilimia 51 mwaka 2015 hadi asilimia 81 mwaka 2022. Amesema uzoefu huo unaonesha kuwa uwekezaji katika miradi inayotekelezeka na inayoweka ustawi wa watu mbele unaweza kugeuza ahadi kuwa matokeo yanayoonekana na kupimika. Kwa msingi huo, amesema Rais Samia Suluhu Hassan alikubali kuwa kinara wa masuala ya Afya ya Mama na Mtoto kwa niaba ya Umoja wa Afrika. Mhe. Ndejembi amesema chini ya uongozi huo, Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama kwa asilimia 80 ndani ya kipindi cha miaka saba, akisisitiza kuwa nchi hiyo inalenga kufikia malengo ya “Sifuri Tatu” (Three Zeros) . Malengo hayo ni kutokuwepo kwa vifo vya mama na mtoto vinavyoweza kuzuilika, kutokuwepo kwa uzazi unaofanyika majumbani na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo. Amesema Afrika inaweza kufikia malengo hayo, lakini inahitaji uongozi thabiti wa kisiasa, rasilimali fedha za kutosha na ushirikiano imara zaidi kutoka kwa jumuiya ya kimataifa. TANZANIA YATAKA MAGEUZI YA MFUMO WA FEDHA DUNIANI Tanzania pia imesisitiza umuhimu wa nchi zinazoendelea kupewa sauti kubwa zaidi katika taasisi na mifumo ya kimataifa inayofanya maamuzi ya kifedha yanayoathiri uchumi na maendeleo yake ya muda mrefu. Mhe. Ndejembi amesema Tanzania imewasilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kama msingi wa kujenga uchumi jumuishi, shindani na unaoweza kustahimili misukosuko, kupitia uwekezaji katika watu, miundombinu yenye tija, teknolojia, ubunifu, wanawake na vijana. Amesema mageuzi katika mfumo wa fedha wa kimataifa ni muhimu ili nchi zinazoendelea ziweze kupata rasilimali zinazohitajika kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Ametaja umuhimu wa kuongeza mikopo yenye masharti nafuu, kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi, kurahisisha upatikanaji wa fedha za maendeleo na tabianchi, pamoja na kuongeza ushiriki wa nchi zinazoendelea katika maamuzi ya kifedha duniani. TABIANCHI, NISHATI SAFI Katika eneo la mabadiliko ya tabianchi, Tanzania imeeleza wasiwasi kuhusu pengo lililopo kati ya kiwango cha uzalishaji wa gesi chafuzi duniani na fedha zinazotolewa kusaidia nchi zinazoathirika kukabiliana na madhara yake. Tanzania imesisitiza kuwa nchi zinazochangia kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa gesi chafuzi zinapaswa kubeba wajibu mkubwa zaidi katika kugharamia hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Katika mkakati wake wa mpito kuelekea nishati safi, Tanzania imetaja Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, miradi ya nishati ya jua na upepo yenye jumla ya megawati 650, pamoja na mipango ya kuzalisha megawati 130 za nishati ya jotoardhi. Pia, Tanzania imeeleza uwekezaji katika reli ya umeme na lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia hadi kufikia asilimia 80 ya kaya ifikapo mwaka 2034. TANZANIA YAPINGA VIKWAZO VYA UPANDE MMOJA Katika diplomasia ya kimataifa, Tanzania imepinga matumizi ya vikwazo vya upande mmoja vinavyowekwa na baadhi ya mataifa dhidi ya mataifa mengine, ikisema hatua hizo zinaweza kudhoofisha mamlaka ya nchi, kuathiri maendeleo na kupunguza uwezo wa wananchi kunufaika kikamilifu na haki zao. Tanzania imeeleza mshikamano wake na Cuba, Zimbabwe na mataifa mengine yanayokabiliwa na vikwazo hivyo, huku ikitoa wito wa kuchukuliwa hatua za makusudi kuelekea kuondolewa kwa vikwazo bila masharti. TANZANIA YATOA WITO WA AMANI GAZA Kuhusu hali ya Gaza na Mashariki ya Kati, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuwalinda raia, kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia wanaohitaji bila vikwazo na kurejesha diplomasia kuwa njia kuu ya kutafuta amani ya kudumu. Kwa ujumla, ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeunganisha ajenda ya maendeleo ya Taifa na hoja pana kuhusu nafasi ya Afrika katika mfumo wa kimataifa. Tanzania imesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa haupaswi kuwa jukwaa linaloakisi pekee uwiano wa nguvu duniani, bali taasisi inayosimamia haki, mshikamano, usawa na maendeleo kwa mataifa yote. Msimamo huo unaweka bayana ajenda ambayo Tanzania inalenga kuibeba katika safari yake ya kuwania nafasi ya uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029–2030; kuimarisha sauti ya Afrika, kuzuia migogoro, kutetea suluhu za amani na kusukuma mageuzi ya mfumo wa kimataifa ili uwe na uwakilishi wenye uwiano zaidi.
Wed, 23 Sep 2026 07:41:37 +0000Page 1115 of 1118 · 22344 stories